KATIBU MKUU UJENZI AKAGUA UKARABATI NYUMBA ZA TBA DODOMA.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mbunifu Majengo Elius Mwakalinga ametembelea na kukagua ukarabati unaofanywa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika nyumba za Serikali mkoani Dodoma na kuridhika na maendeleo ya ukarabati huo.
Katibu Mkuu Mwakalinga, amekagua ukarabati katika nyumba za Serikali zilizopo eneo la Kisasa Jijini Dodoma. Akielezea ukarabati huo, Meneja wa TBA mkoa wa Dodoma, Mbunifu Majengo Victor Baltazar amesema, sehemu zinazofanyiwa ukarabati zinahusisha na kuondoa madirisha yaliyokuwepo na kuweka mapya, kupaka rangi, kujenga uzio, kurekebisha paa, mfumo wa maji safi na taka pamoja mazingira ya nje.
Aidha Katibu Mkuu Mwakalinga ameridhishwa na ukarabati huo unaoendelea katika eneo hilo la Kisasa na kuahidi kuendelea na ziara hiyo tena katika nyumba nyingine za ghorofa ambazo ukarabati wake unaendelea katika eneo la Area D.
TBA ilianza ukarabati wa nyumba za Serikali katika mkoa wa Dar es salaam, sasa Dodoma na zoezi hilo litaendelea katika mikoa mbalimbali nchini kuhakikisha kwamba nyumba hizo zinakuwa katika mazingira mazuri ya kuishi.