MTENDAJI MKUU TBA ARCH. KONDORO AKABIDHIWA TUZO NA CHETI CHA USHIRIKI MAONESHO YA MADINI NA WIKI YA WAHANDISI

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Daudi Kondoro, amekabidhiwa tuzo na cheti kufuatia ushiriki wa TBA katika maonesho yaliyofanyika Mkoani Geita na jijini Dar es Salaam.
Makabidhiano hayo yamefanyika Oktoba 8, 2025 katika Ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi ndogo za TBA Makao makuu jijini Dar es Salaam, ambapo Kaimu Meneja wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko, Bw. Adam Mwingira amekabidhi tuzo na cheti zilizopokelewa katika Maonesho hayo.
Katika Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika Mkoani Geita, TBA iliibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa taasisi za umma na pia kutunukiwa tuzo ya shukrani kutokana na mchango wake wa udhamini wa maonesho hayo.
Vilevile, katika Maonesho ya Wiki ya Wahandisi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Mlimani City, TBA ilipokea cheti cha ushiriki, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake katika kuunga mkono taaluma ya uhandisi nchini.
Tuzo na cheti hicho ni uthibitisho wa dhamira ya wakala kuendelea kutoa huduma bora katika sekta ya ujenzi pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa makazi bora nchini.