DC MKALAMA AIPONGEZA TBA KWA UBUNIFU NA UTEKELEZAJI BORA WA MIRADI

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Moses Mashali, amepongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa utekelezaji mzuri wa miradi mikubwa ya ujenzi, ukiwemo ujenzi wa Mji wa Serikali uliopo Mtumba, Jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la TBA katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, Dodoma, Mhe. Mashali amesema amevutiwa na ubunifu unaoonyeshwa na wakala huo hususan katika sekta ya ujenzi wa makazi na miundombinu ya kisasa.
“Nimefurahishwa sana na mpango wa ushirikiano baina yenu na sekta binafsi. Huu ni mwendelezo chanya ambao utaimarisha maendeleo ya sekta ya nyumba na makazi kwa wananchi. Pia nimeona kazi nzuri ya ubunifu wa majengo katika Mji wa Serikali mazingira yake ni ya kupendeza na yenye viwango,” amesema Mhe. Mashali.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa wito kwa taasisi na mashirika mengine kufika katika banda hili ili kujifunza kutoka kwa TBA, akieleza kuwa ni mfano bora wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa weledi na ubunifu wa hali ya juu.
TBA inashiriki maonesho ya Nanenane mwaka huu katika viwanja viwili: Nzuguni, Dodoma na Ngongo, mkoani Lindi, ambapo imeendelea kuonesha mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati inayochochea maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.