KATIBU TAWALA GEITA AWAALIKA WAWEKEZAJI KUSHIRIKIANA NA TBA KATIKA MIRADI YA UWEKEZAJI
Leo, Septemba 30, 2026, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamedi J. Gombati, ametembelea Banda la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini 2026, na kuipongeza TBA kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali mikubwa mkoani Geita.
Gombati amewataka wananchi na wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo katika maeneo ya TBA yaliyoandaliwa kwa ajili ya uwekezaji, akitaja Misheni Kota na eneo la Msikitini kuwa maeneo yenye fursa za uwekezaji kupitia Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP).
Amesema hatua hiyo inaendana na dhamira ya Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha, amempongeza Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, kwa kuendelea kuwakaribisha wananchi na wawekezaji kushirikiana na TBA katika kuyaendeleza maeneo hayo pamoja na maeneo mengine yanayosimamiwa na TBA.
Pia Gombati ameipongeza TBA kwa kazi nzuri katika huduma za Ushauri (Consultancy) na Ujenzi, akitaja miradi ya Rest House, Ofisi na makazi ya Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, pamoja na usimamizi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na nyumba ya makazi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Kutokana na uzoefu huo, amezishauri taasisi za Umma na Binafsi kutumia huduma za TBA katika utekelezaji wa miradi ya Ujenzi, akieleza kuwa Wakala una uwezo mkubwa wa kutekeleza kazi hizo kwa ufanisi, Huku akitolea mfano wa utekelezaji wa Miradi wa TBA katika Mkoa wa Geita
TBA inaendelea kuwakaribisha wananchi na wawekezaji kupata taarifa kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji, ikiwemo nyumba zinazopangishwa na kuuzwa, pamoja na maeneo na viwanja vinavyohitaji kuendelezwa kupitia ubia.