MHE. CHALAMILA AITAKA TBA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEKEZAJI.
Dar es Salaam, Oktoba 23, 2026.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ameitaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kutumia kikamilifu fursa za uwekezaji katika maeneo inayoyasimamia ili kuongeza thamani ya mali za Serikali, kukuza uchumi na kuboresha huduma kwa wananchi.
Mhe. Chalamila alitoa maelekezo hayo alipotembelea Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya TBA jijini Dar es Salaam, ambapo alizungumza na Menejimenti na watumishi kuhusu matumizi bora ya rasilimali za Wakala kwa manufaa ya Serikali na umma.
Katika ziara hiyo, alitembelea maeneo ya TBA yaliyopo Kinondoni Manyanya na Ilala Kota, akipata maelezo kuhusu hali ya maeneo hayo na mipango ya kuyaendeleza. Alibainisha fursa za uwekezaji, zikiwemo majengo makubwa ya biashara, maegesho ya magari ya kibiashara, vituo vya michezo na kumbi za kisasa za mikutano kwa Taasisi, mashirika na Balozi.
Aidha, alipendekeza ujenzi wa majengo yenye matumizi mchanganyiko ya makazi na biashara, pamoja na vituo vinavyotoa huduma mbalimbali katika eneo moja. Alieleza kuwa uwekezaji huo unaweza kuongeza thamani ya maeneo, kupanua ajira na kuongeza mapato kupitia matumizi bora ya mali za Serikali.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TBA, FRV. Said R. Mndeme (ndc), alimkaribisha Mkuu wa Mkoa na kueleza kuhusu maeneo yaliyotembelewa, maeneo mengine ya Wakala na mikakati ya kuyaendeleza kwa kuzingatia mahitaji ya soko na tija ya kiuchumi.
Mndeme alieleza kuwa TBA inaendelea kutathmini fursa za uwekezaji, ikiwemo kushirikiana na sekta binafsi kupitia Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ili kuharakisha utekelezaji wa miradi na kuongeza thamani ya rasilimali za Serikali.
Aidha, aliahidi kuyafanyia kazi maelekezo na ushauri wa Mkuu wa Mkoa na kuzingatia katika mipango ya maendeleo ya maeneo hayo, kwa mujibu wa taratibu na miongozo ya uwekezaji.
Ziara hiyo imelenga kuimarisha ushirikiano kati ya TBA na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika kuendeleza fursa za uwekezaji na kuongeza tija ya mali za Serikali kwa maendeleo ya Dar es Salaam.