Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

HAKIKISHENI MNAIPITIA DIRA YA TAIFA 2050 - ARCH. KONDORO

Imewekwa: 29 August, 2025
HAKIKISHENI MNAIPITIA DIRA YA TAIFA 2050 - ARCH. KONDORO

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Daud Kondoro, amewataka watumishi wote wa TBA kuhakikisha wanaipitia Dira ya Taifa ya mwaka 2050, ili kujiandaa na kupanga mikakati ya namna ya kuitekeleza kupitia majukumu ya taasisi.

Arch. Kondoro ametoa wito huo wakati akizindua kikao cha Baraza la Wafanyakazi (TUGHE) kilichofanyika katika ofisi ndogo za Makao Makuu ya TBA jijini Dar es Salaam. Amesema ni wajibu wa kila mtumishi kuielewa dira hiyo kwa kuwa ndiyo mwongozo wa maendeleo ya taifa kwa kipindi kijacho.

“Kila mtumishi wa TBA anapaswa kuifahamu na kuielewa Dira ya Taifa ya 2050. Hii itatupa mwongozo wa namna bora ya kushiriki katika utekelezaji wake kupitia miradi ya ujenzi na huduma tunazotoa,” amesema Kondoro.

Kikao hicho kililenga kujadili mwenendo wa wanachama wa chama hicho pamoja na kufanya tathmini ya namna chama kinavyokabiliana na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.

Mbali na ajenda hizo, wanachama wa TUGHE walipata elimu ya uwekezaji kutoka kwa wataalamu wa Mfuko wa Uwekezaji wa UTT, ambapo walihimizwa kutumia fursa hiyo kuongeza kipato chao ili kupunguza changamoto za maisha.

Aidha, wanachama hao walipata elimu ya afya kutoka kwa daktari wa Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Ukimwi (TACAIDS). Elimu hiyo imelenga kuwajengea uelewa wa namna ya kujilinda na kuzingatia afya zao ili wawe na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.