Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA MRADI WA MAKAZI WA CANADIAN MASAKI

Imewekwa: 30 March, 2026
KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA MRADI WA MAKAZI WA CANADIAN MASAKI

Machi 24, 2026 — Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa nyumba za makazi ya kibiashara wa Canadian Masaki unaotekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo imefanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani ya TBA, ikiwa ni sehemu ya juhudi ya taasisi  kuimarisha uwekezaji katika sekta ya makazi.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Masanja Kadogosa, ameipongeza TBA kwa utekelezaji wa mradi huo kwa ubora wa hali ya juu, huku ikizingatia mahitaji ya kisasa ya makazi.

Aidha, Mhe. Kadogosa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa mradi huo, akibainisha kuwa hatua hiyo inaakisi dhamira ya serikali ya kuboresha sekta ya makazi nchini.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo ameipongeza TBA kwa kuanza mchakato wa utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi huo, ambapo nyumba zitauzwa kwa mfumo wa Pre-Selling. Amesema mfumo huo wa kisasa utasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi pamoja na kuimarisha mapato ya taasisi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amesema miradi hiyo ina tija na itasaidia kuongeza mapato ya taasisi pamoja na kupunguza utegemezi wa kifedha kutoka serikalini.