KATIBU MKUU WA KILIMO AWAHIMIZA WADAU KUITUMIA TBA KATIKA MIRADI YA UJENZI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, amezihimiza taasisi za serikali na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo kuitumia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi kutokana na ubora wa huduma zinazotolewa na wakala.
Mweli ametoa wito huo leo Agosti 6, 2026, alipotembelea banda la TBA katika Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Amesema Wizara ya Kilimo imekuwa ikishirikiana na TBA katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi, ikiwemo ujenzi wa maghala ya kuhifadhia chakula na ofisi za wizara hiyo.
“Tumefanya kazi nyingi na TBA. Wamejenga maghala ya kuhifadhia chakula na ofisi za Wizara ya Kilimo. Nawashauri wadau wengine wa kilimo wasisite kuitumia TBA katika kutekeleza miradi yao ya ujenzi,” amesema Mweli