RC SINYAMULE AIPONGEZA TBA KWA MIRADI YA MAENDELEO NANENANE NZUGUNI, DODOMA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Staki Sinyamule, ametembelea banda la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo, Mhe. Sinyamule alipata fursa ya kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa na TBA kote nchini, ikiwemo ujenzi wa Mji wa Serikali uliopo Mtumba, jijini Dodoma, pamoja na ujenzi wa vihenge na maghala ya kisasa ya kuhifadhia chakula katika mikoa minane ambayo ni Dodoma, Shinyanga, Manyara, Njombe, Songwe, Rukwa, Katavi na Ruvuma.
Pia, amejionea utekelezaji wa ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha vifaranga wa samaki wa maji chumvi katika maeneo ya Ruvula Msimbati mkoani Mtwara na Kunduchi jijini Dar es Salaam.
Miradi mingine aliyojionea ni pamoja na ujenzi wa soko la mnada wa pili wa mifugo katika eneo la Buzirayombo, mkoani Geita, pamoja na mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba 3,500 za watumishi wa umma katika eneo la Nzuguni, jijini Dodoma.
Baada ya kutembelea banda hilo, Mhe. Sinyamule ameonyesha kuridhishwa kwake na juhudi kubwa zinazofanywa na TBA katika kuleta mageuzi ya sekta ya ujenzi na kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati.
Katika maonesho hayo, TBA pia inatumia fursa hiyo kuwaalika wawekezaji kuingia ubia katika miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi na biashara ili kuharakisha upatikanaji wa makazi bora na ya kisasa kwa Watanzania.