Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

BODI YA USHAURI TBA YAPITISHA MPANGO MKAKATI MPYA, YAKAGUA MRADI WA NYUMBA MAGOMENI KOTA

Imewekwa: 26 July, 2026
BODI YA USHAURI TBA YAPITISHA MPANGO MKAKATI MPYA, YAKAGUA MRADI WA NYUMBA MAGOMENI KOTA

Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imepitisha Mpango Mkakati wa TBA wa miaka mitano wa 2026/27–2030/31 pamoja na Mpango wa Manunuzi wa mwaka wa fedha 2026/27, hatua inayolenga kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Wakala na kufanikisha malengo yake ya kimkakati.

Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Bodi kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TBA, Dkt. Lauren Ndumbaro, kilichofanyika Julai 24, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Ndogo za TBA, jijini Dar es Salaam.

Sambamba na hilo, Leo Julai 25, 2026 Bodi hiyo pia imefanya ziara ya kukagua maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Nyumba za Makazi wa Magomeni Kota, Dar es Salaam ili kujionea hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo.

Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi, Meneja wa TBA Mkoa wa Dar es Salaam, Arch. Benard Mayemba, amesema ujenzi umefikia hatua za mwisho na kwamba kazi zilizobaki zinatarajiwa kukamilika kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa.

Akizungumza baada ya ukaguzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Lauren Ndumbaro, amesema Bodi imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi na kusisitiza kuwa mradi huo ni utekelezaji wa sera za Serikali za kuboresha makazi ya wananchi.

"Leo tumetembelea mradi huu unaofadhiliwa na Serikali na tumeridhishwa na maendeleo yake. Baadhi ya majengo yamefikia hatua za mwisho za ujenzi, na tunatarajia ifikapo Oktoba mwaka huu jengo moja litakuwa limekamilika na tayari kwa matumizi"  amesema Dkt. Ndumbaro.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miliki wa TBA, FRV. Said R. Mndeme (NDC), amesema eneo la Magomeni Kota lina ukubwa wa hekari 32, ambapo awamu ya kwanza ya mradi ilihusisha ujenzi wa majengo matano ya ghorofa yaliyotoa makazi kwa wakazi 644 na tayari yamekamilika.

Ameeleza kuwa kwa sasa TBA inaendelea na awamu ya pili ya mradi, ambayo itahusisha ujenzi wa majengo mengine matano yatakayokuwa na uwezo wa kuhudumia familia 80. Hadi sasa, majengo mawili yenye uwezo wa kuchukua familia 32 yamekamilika na yapo katika hatua za mwisho za maandalizi kabla ya kuanza kutumika.

FRV. Mndeme amesema ziara ya Bodi ya Ushauri ilijikita katika ukaguzi wa majengo hayo mawili, ambayo yamefikia hatua za mwisho za ujenzi.

Aidha, amewahimiza wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo katika eneo lililosalia la Magomeni Kota kwa kuwekeza kupitia ubia na TBA, ameeleza kuwa eneo hilo lina miundombinu muhimu na mazingira rafiki kwa maendeleo ya miradi ya makazi na uwekezaji.

slot gacor