Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

KAMATI YA UKAGUZI TBA YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI DODOMA

Imewekwa: 21 August, 2025
KAMATI YA UKAGUZI TBA YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI DODOMA

Kamati ya Ukaguzi ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imefanya ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa jijini Dodoma, ikiwemo ukarabati wa nyumba za makazi ya watumishi wa umma, nyumba za viongozi eneo la Kisasa, jengo la Mionzi katika Hospitali ya Benjamini Mkapa, pamoja na miradi ya ushauri katika Mji wa Serikali Mtumba.

Miradi mingine iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba 3,500 za makazi katika eneo la Nzuguni pamoja na mitambo ya ujenzi inayomilikiwa na TBA.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bi. Juliana Melo, aliipongeza TBA kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwataka kuhakikisha changamoto zote zilizobainishwa zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Naye Mjumbe wa Kamati hiyo, PQs. Abdon Mhando, alisema utekelezaji wa miradi hiyo ni wa kuridhisha na unatia moyo kwani ushauri unaotolewa umekuwa ukifanyiwa kazi ipasavyo. Ameongeza kuwa changamoto zilizopo ni za kawaida katika sekta ya ujenzi na amesisitiza kuridhishwa kwake na kasi ya utekelezaji wa miradi ya TBA.

Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Mkoa, Mhandisi George Chaula, mwakilishi wa TBA aliwahakikishia wajumbe wa kamati hiyo kuwa taasisi hiyo imejipanga kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na kuendeleza ubora katika miradi yake.