“Ubunifu na mabadiliko ya Teknolojia, chachu katika kuleta usawa wa kijinsia ni kauli mbiu iliyobeba maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofikia kilele chake Machi 8, 2023. Maadhimisho hayo yaliambatana na maandamano yaliyofanyika katika mikoa mbalimbali nchini pamoja na maonesho ya bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa na wanawake wajasiriamali.
Wafanyakazi wanawake wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) waliungana na wanawake wengine dunia kusherehekea maadhimisho hayo ambayo yalifanyika katika mikoa mbalimbali nchini.
Viongozi mbalimbali walioudhuria sherehe hizo waliwapongeza wanawake na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuendana na mahitaji ya teknolojia. Akizungumza wakati wa sherehe hizo katika viwanja vya Mnazi mmoja Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla ametoa ujumbe kwa wanawake wa mkoa wa Dar es Salaam kuwa Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa mwanamke hivyo ni vyema wanawake wakatumia fursa zinazopatikana katika jamii kwa kufanya ubunifu unaoendana na teknolojia ya sasa.
Awali Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro alitoa baraka zake kwa wanawake wa TBA kabla ya kuanza kwa maandamo hayo katika ofisi za Wakala jijini Dar es Salaam. Pia Arch. Kondoro aliwapongeza wanawake wa TBA kwa kazi nzuri wanazozifanya kila mmoja katika eneo lake ambazo zimekuwa chachu ya mafanikio ya Wakala na taifa kwa ujumla. "Kama kauli mbiu yenu inavyosema Ubunifu na mabadiliko ya Teknolojia, chachu katika kuleta usawa wa kijinsia hivyo kila mnachokifanya hapa TBA, kinaonekanakuwa na tija kwa maendeleo ya taasisi yetu" aliongeza Arch. Kondoro.
Wanawake wa TBA wamemshukuru Mtendaji Mkuu pamoja na menejimenti ya TBA kwa kuwawezesha kutekekeza majukumu yao katika maeneo mbalimbali.