MTENDAJI MKUU WA TBA AWATAKA WATUMISHI WA SHINYANGA KUONGEZA BIDII KATIKA USIMAMIZI WA MIRADI NA UKUSANYAJI WA MAPATO
Shinyanga, Novemba 16, 2026.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), FRV. Said R. Mndeme (ndc), amewataka watumishi wa TBA Mkoa wa Shinyanga kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na mshikamano ili kuhakikisha wanafikia malengo ya Wakala katika usimamizi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya majengo inayotekelezwa kwa dhamana ya Serikali.
Mtendaji Mkuu ametoa rai hiyo Novemba 16, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi inayoendelea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambapo alipata fursa ya kukutana na watumishi hao na kusikiliza changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.
Amewasisitiza watumishi hao kuendelea kuimarisha usimamizi wa miradi pamoja na kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na rasilimali za TBA zilizopo mkoani humo.
_“Endeleeni kuimarisha usimamizi wa miradi yetu hapa Shinyanga. Kufanya hivyo kutachochea ukusanyaji wa mapato na kuongeza mchango wa Mkoa katika kufikia malengo ya Wakala, kama ilivyo kwa mikoa mingine ikiwemo Dar es Salaam, Arusha na Dodoma,”_alisisitiza Mtendaji Mkuu.
Kwa upande wao, watumishi wa TBA Mkoa wa Shinyanga wamemshukuru Mtendaji Mkuu kwa ziara hiyo na kuahidi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na ufanisi ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali pamoja na Wakala.