TBA YAFANYA UKAGUZI WA MAENEO YAKE KWA AJILI YA KUYAENDELEZA

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeanza zoezi maalum la ukaguzi wa maeneo yake ambayo hayajaendelezwa, likianzia katika Wilaya ya Kigamboni, mkoani Dar es Salaam.
Zoezi hilo limeongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Miliki wa TBA, FRV Said Mndeme (ndc), akishirikiana na watumishi kutoka Idara ya Miliki Makao Makuu pamoja na wenzao wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mndeme amesema lengo kuu ni kuhakikisha maeneo yanayomilikiwa na TBA yanafanyiwa usafi, yanaainishwa kisheria kupitia usajili sahihi na kuanza taratibu za kuyapanga kwa ajili ya maendeleo.
“ Ni wajibu wetu kuyatambua maeneo yote na kuyahifadhi ipasavyo ili yaweze kutumika kwa faida na miradi iliyokusudiwa,” amesema Mndeme.
Aidha, amebainisha kuwa ukaguzi huo ni endelevu na utafanyika katika mikoa yote nchini ili kubainisha na kuthibitisha umiliki wa maeneo yote ya TBA.