Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

TBA YAENDELEA KUTOA NAFASI ZA MAFUNZO KWA VITENDO KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU

Imewekwa: 25 February, 2026
TBA YAENDELEA KUTOA NAFASI ZA MAFUNZO KWA VITENDO KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeeleza kuwa utaendelea kutoa fursa za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali wanaoomba kufanya mafunzo hayo katika taasisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya kuchangia maendeleo ya taaluma na kuongeza uzoefu kwa vijana wanaojiandaa kuingia katika soko la ajira.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu, Februari 23, 2026, na Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, wakati akizungumza katika mkutano wa wanafunzi wa Ndaki ya Uhandisi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Arch. Kondoro amesema TBA imekuwa ikitoa ushirikiano wa kutosha kwa wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo ili kuwasaidia kufanikisha mahitaji yao ya kitaaluma, na kwamba taasisi hiyo itaendelea kudumisha utaratibu huo.

“TBA imekuwa ikiwapa nafasi wanafunzi wanaoomba kufanya mafunzo kwa vitendo, na tumekuwa tukiwapatia ushirikiano unaohitajika ili kufanikisha malengo yao ya kujifunza. Tutaendelea kufanya hivyo,” amesema.

Aidha, amewahimiza wataalamu wa sekta ya ujenzi kujisajili katika Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) ili kutambulika rasmi kitaaluma, akibainisha kuwa TBA iko tayari kushirikiana na wataalamu wote waliosajiliwa na bodi hiyo.

Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ukihusisha taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa ujenzi Mhe. Abdallah Ulega.