TBA YAKUTANA NA CRDB NA ABSA KUJADILI FURSA ZA UFADHILI WA MIRADI YA KIMKAKATI
Dar es Salaam, Novemba 19, 2026
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), FRV. Said R. Mndeme (ndc), pamoja na Menejimenti ya Wakala, leo amekutana na kufanya vikao tofauti na wawakilishi wa Benki ya CRDB na Benki ya Absa katika Ofisi za TBA, Dar es Salaam, kwa lengo la kujadili fursa za ushirikiano wa kifedha na upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya Wakala.
Akifungua vikao hivyo, Mtendaji Mkuu wa TBA, FRV. Said R. Mndeme (ndc), amewakaribisha wawakilishi hao na kuwafahamisha kuhusu majukumu ya Wakala, fursa za uwekezaji zilizopo pamoja na miradi ya kimkakati inayotarajiwa kutekelezwa, akieleza umuhimu wa ushirikiano na taasisi za kifedha katika kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika vikao hivyo, TBA imewasilisha mipango ya maendeleo ya miradi ya Magomeni Kota na Canadian Village, Masaki, ikiwemo mikakati ya utekelezaji, fursa za uwekezaji na uwezekano wa kutumia mifumo mbalimbali ya ufadhili, pamoja na utaratibu wa mauzo ya awali (*Pre-sale*) ya nyumba zitakazojengwa katika miradi hiyo.
Akizungumza katika kikao na TBA, mwakilishi wa Benki ya CRDB, RM. Mike Kasungu, ameipongeza TBA kwa kuunda timu ya kuratibu ushirikiano huo, akieleza imani yake kuwa ushirikiano wa karibu utawezesha kufikiwa kwa malengo ya miradi husika. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia Green Financena Sustainability katika utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha uwekezaji endelevu na wenye tija ya muda mrefu.
Kwa upande wa Benki ya Absa, Bi. Nellyana Mmanyi amesisitiza umuhimu wa maandalizi ya nyaraka za msingi za miradi na uratibu wa karibu kati ya timu za TBA na benki, akieleza kuwa hatua hizo ni muhimu katika kuwezesha tathmini ya fursa za ufadhili na kuharakisha utekelezaji wa hatua zinazofuata.
Mikutano hiyo ni sehemu ya juhudi za TBA za kuimarisha ushirikiano na taasisi za kifedha, kuongeza upatikanaji wa mitaji na kuvutia uwekezaji katika miradi ya kimkakati. Ushirikiano huo unatarajiwa kuchochea utekelezaji wa miradi ya majengo, kuongeza upatikanaji wa makazi na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Taifa.