TBA YAKABIDHI TUZO NNE ZILIZOPOKELEWA, MTENDAJI MKUU ATOA MAELEKEZO YA KUIMARISHA UTENDAJI
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umekabidhi tuzo nne zilizopokelewa kutokana na mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake. Hafla hiyo imefanyika leo, Novemba 05, 2026, katika Ukumbi wa Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya TBA jijini Dar es Salaam, ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wa TBA, FRV. Said R. Mndeme (ndc).
Tuzo hizo ni Tuzo ya Mshindi wa Pili kwa Taasisi za Umma – Real Estate Exhibitor katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba); Tuzo ya Mshindi wa Pili kwa Taasisi za Umma katika Maonesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita; Tuzo ya Mdhamini wa Maonesho hayo na Tuzo ya AQIPT Training Partners Awards iliyotolewa na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).
Akizungumza katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu FRV. Said Mndeme (ndc) ameipongeza Menejimenti na watumishi kwa mafanikio hayo, akibainisha kuwa ni matokeo ya mipango madhubuti, maandalizi, ushirikiano na utekelezaji wa majukumu kwa weledi na ubunifu.
Katika maelekezo yake, Mtendaji Mkuu ameitaka Menejimenti kuhakikisha kila Kurugenzi, Kitengo na Sehemu inatekeleza majukumu kwa kuzingatia malengo, kuongeza ubunifu, kuimarisha usimamizi na kuweka mkazo katika matokeo yanayopimika.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa mshikamano, ushirikiano, kubadilishana uzoefu, kutatua changamoto kwa wakati na kuthamini mchango wa kila mtumishi. Ameeleza kuwa tuzo hizo ni mafanikio ya kujivunia, lakini ni muhimu zaidi kudumisha mafanikio hayo na kuyatumia kufikia viwango vya juu vya utendaji.
Aidha, FRV. Mndeme amewahimiza watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uwajibikaji na kujituma ili TBA iendelee kupata mafanikio makubwa na kuongeza thamani kwa taasisi na wadau wake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi, Bi. Amina Lumuli, amemshukuru Mtendaji Mkuu kwa pongezi, maelekezo na mwongozo alioutoa kwa niaba ya Menejimenti na watumishi wote. Ameahidi kuwa Menejimenti itayafanyia kazi maelekezo hayo kwa vitendo kwa kuhakikisha yanaingizwa katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ili kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi wa Wakala.