TBA YAELEZA MAFANIKIO YA MIRADI YA KILIMO, YATOA WITO KWA WAWEKEZAJI
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa majengo ya Serikali katika sekta tofauti, ikiwemo miradi ya kilimo, afya na maji
Meneja wa TBA Mkoa wa Dodoma, QS. Emmanuel Wambura, amesema hayo wakati akizungumza katika banda la TBA kwenye Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni, Dodoma.
QS. Wambura amesema TBA imekuwa mshiriki muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya sekta ya kilimo nchini, ikiwemo ujenzi wa ofisi za Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), ofisi za Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, vihenge vya kisasa vya kuhifadhia chakula katika mikoa nane pamoja na maghala ya kuhifadhia chakula.
Ametaja miradi mingine kuwa ni ujenzi wa ofisi za Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na jengo la Ofisi ya Wizara ya Kilimo lililopo katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.
"Pamoja na miradi ya kilimo, TBA pia tumeshiriki katika miradi ya afya kwa kujenga baadhi ya vituo vya afya hapa Dodoma, Hospitali ya Uhuru na jengo la Wizara ya Afya. Aidha, TBA imevuka mipaka ya nchi kwa kushiriki katika ujenzi wa baadhi ya majengo ya balozi za Tanzania zilizoko nje ya nchi," amesema Qs. Wambura.
Kwa upande wa uwekezaji, Meneja Wambura ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kushiriki katika miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) inayotekelezwa na TBA.
Amesema TBA imetenga eneo la ukubwa wa hekari 630 katika eneo la Nzuguni, Dodoma, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ubia, ambapo maendeleo ya awali tayari yameanza kupitia ujenzi wa nyumba za makazi 3,500 unaoendelea katika eneo hilo.
"Dodoma tuna eneo lenye ukubwa wa hekari 630 ambalo limetengwa kwa ajili ya miradi ya ubia. Tayari tumeanza kuliendeleza kwa kuanza ujenzi wa nyumba za makazi 3,500, hivyo tunawakaribisha wawekezaji waje tushirikiane kuendeleza eneo hili," amesema Qs. Wambura.
TBA inashiriki Maonesho ya Nanenane mwaka huu kwa lengo la kuonyesha huduma zake, miradi inayotekeleza pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana kupitia wakala huu.