Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

TBA YAWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEKEZAJI KUPITIA PPP KATIKA MAENEO 38 YALIYOIVA TANZANIA BARA

Imewekwa: 05 October, 2026
TBA YAWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEKEZAJI KUPITIA PPP KATIKA MAENEO 38 YALIYOIVA TANZANIA BARA

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Ujenzi, inayoshiriki katika Maonesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.

Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja Mawasiliano na Masoko TBA, Bw. Adam Mwingira, amesema TBA inatoa fursa mbalimbali za uwekezaji kwa wadau na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Amesema, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umetangaza takribani maeneo 38 yaliyoiva kwa ajili ya uwekezaji katika takribani mikoa 20 ya Tanzania Bara. Maeneo hayo yamefanyiwa upembuzi yakinifu (Feasibility Study) pamoja na utafiti wa soko (Market Survey), ambao umeonesha kuwa yana fursa nzuri za uwekezaji na mahitaji makubwa ya soko. Aidha, maeneo hayo yamezungukwa na miundombinu mbalimbali kama vile barabara za kisasa, maji, umeme na huduma wezeshi zinazochangia kuongeza faida kubwa kwa wawekezaji. 

Hata hivyo, mkoani Geita, TBA ina maeneo mawili yaliyoiva kwa uwekezaji ambayo ni eneo la Mission Kota lenye ukubwa wa takribani mita za mraba 10,620, huku eneo la pili la Msikitini likiwa na ukubwa wa takribani futi za mraba 24,330.

Maeneo haya yameiva kwa ajili ya uwekezaji na miundombinu inayorahisisha shughuli za uwekezaji, ikiwemo barabara na miundombinu mingine inayoweza kuongeza thamani ya uwekezaji.

Mbali na Geita, TBA ina maeneo mengine yaliyoiva kwa ajili ya uwekezaji katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Simiyu, Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Tabora, Songwe na mikoa mingine katika Tanzania Bara.

TBA inawakaribisha wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi kushirikiana na Wakala kupitia utaratibu wa ubia kati ya Serikali na sekta binafsi, yaani Public-Private Partnership (PPP).

Kupitia ushirikiano huo, mwekezaji anaweza kutumia fursa zilizopo katika maeneo haya kwa kuzingatia mahitaji ya soko, mazingira ya eneo husika pamoja na matokeo ya upembuzi yakinifu na tafiti za soko zilizofanyika.

 Maeneo haya yako tayari kwa ajili ya uwekezaji na yanatoa fursa mbalimbali kwa wawekezaji wanaotafuta maeneo yenye uwezo wa kuendeleza miradi yenye tija.

Aidha, TBA inawakaribisha kutembelea Banda lake kwenye Maonesho ya 9 ya Teknolojia ya Madini katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Bombambili Mkoani Geita ili kupata maelezo zaidi na kuona fursa mbalimbali za uwekezaji zinazotolewa na TBA.

slot gacor