TBA YAWEKA MSINGI IMARA WA UTAWALA BORA WA UNUNUZI WA UMMA
Leo Februari 24, 2026, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, amefungua rasmi mafunzo ya kimkakati ya Sheria na Kanuni za Ununuzi wa Umma yanayofanyika katika Ukumbi wa Peacock Hotel, Jijini Dar es Salaam. Mafunzo haya ya siku tano yalianza Februari 23 na yanatarajiwa kukamilika Februari 27, 2026.
Katika hotuba yake yenye mwelekeo wa kimkakati, Arch. Kondoro ameweka wazi kuwa TBA inaendelea kujijenga kama taasisi imara inayozingatia uwazi, uwajibikaji na thamani halisi ya fedha za umma. Mafunzo haya yanawaleta pamoja Menejimenti, Bodi ya Zabuni na Kitengo cha Ununuzi na Ugavi (PMU) kwa lengo la kuimarisha uwezo wa taasisi katika kusimamia zabuni, mikataba na huduma kwa viwango vya juu vya kitaaluma.
Akisisitiza umuhimu wa mafunzo hayo, alibainisha kuwa uelewa sahihi wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 na Kanuni zake za mwaka 2024 ni nyenzo muhimu ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi, kuondoa mapungufu ya kiutendaji na kuhakikisha TBA inaendelea kuwa mshauri elekezi na mkandarasi wa kuaminika kitaifa.
Aidha, alitoa pongezi kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa ushirikiano wake katika kutoa mafunzo hayo, akieleza kuwa ushirikiano huo unaimarisha zaidi misingi ya utawala bora na ubora wa huduma ndani ya taasisi.
Kupitia mafunzo haya, TBA inawekeza katika rasilimali watu wake kwa lengo la kujenga mfumo madhubuti wa ununuzi utakaowezesha taasisi kusimamia miradi kwa ufanisi mkubwa, kuzingatia takwa la asilimia 30 kwa makundi maalum na kuendana na dira ya Taifa ya maendeleo 2050 chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan