Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

TBA YAACHA ALAMA YA KIHISTORIA MTUMBA: MCHANGO WAKE WANG’ARA KUELEKEA UZINDUZI WA MJI WA SERIKALI

Imewekwa: 29 October, 2026
TBA YAACHA ALAMA YA KIHISTORIA MTUMBA: MCHANGO WAKE WANG’ARA KUELEKEA UZINDUZI WA MJI WA SERIKALI

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa Mradi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, kupitia ubunifu wa majengo, usimamizi wa ujenzi na huduma za kitaalamu za ushauri elekezi. Mchango huo unaweka alama muhimu katika historia ya maendeleo ya miundombinu ya Serikali, kuelekea uzinduzi rasmi wa Mji huo unaotarajiwa kufanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Oktoba 30, 2026.

Katika Awamu ya Kwanza ya mradi huo, TBA ilibuni majengo 22 ya Wizara na majengo matatu ya taasisi za Serikali, ambazo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, TARURA na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA). Aidha, Wakala ulisimamia ujenzi wa majengo yote ya Wizara katika awamu hiyo na kutekeleza jukumu la Mshauri Elekezi, ukitoa huduma za kitaalamu katika kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa kuzingatia mahitaji yaliyokusudiwa.

Katika Awamu ya Pili, TBA imeendelea kuonesha uwezo wake wa kitaalamu kwa kufanya ubunifu wa majengo 24 ya Wizara na majengo saba ya taasisi za Serikali. Taasisi hizo ni Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Shirika la Posta Tanzania na Commanding Centre.

Aidha, TBA ilitekeleza ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kama Mkandarasi. Jengo hilo limekamilika na tayari limeanza kutumika, likiwa ni sehemu ya miundombinu muhimu inayowezesha shughuli za Serikali kutekelezwa katika mazingira bora ya kazi.

Kukamilika kwa Mji wa Serikali Mtumba ni hatua muhimu katika kuimarisha utendaji wa Serikali, kurahisisha uratibu wa shughuli za kiutawala na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wananchi. Ushiriki wa TBA katika awamu zote mbili unaonesha uwezo, utaalamu na mchango wa Wakala katika kubuni, kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayochochea maendeleo ya Taifa.

slot gacor