TBA YAFUNGUA MILANGO YA USHIRIKIANO WA UWEKEZAJI NA FUJITA CORPORATION YA JAPAN
Dar es Salaam, Novemba 13, 2026.
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeendelea kuimarisha juhudi za kuvutia wawekezaji wa kimataifa kupitia kikao cha mazungumzo ya uwekezaji na kampuni ya Fujita Corporation ya Japan, kilichofanyika katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya TBA, Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa TBA, FRV. Said Mndeme (ndc), aliwakaribisha ujumbe wa Fujita Corporation na kuieleza kampuni hiyo kuwa TBA ni mshirika salama na wa kuaminika kwa uwekezaji, kutokana na kuwa na maeneo ya kimkakati yaliyoiva kwa ajili ya uwekezaji na yenye fursa kubwa za kibiashara.
Aidha, Mtendaji Mkuu aliieleza Fujita Corporation kuwa kampuni yenye uzoefu mkubwa na mafanikio katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi na maendeleo katika nchi na maeneo mbalimbali, Alieleza kuwa kuingia katika makubaliano ya ushirikiano na kampuni hiyo kutakuwa na manufaa makubwa kwa TBA na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Meneja wa Fujita Corporation, Kenya Branch, Kiyoyoshi Kimura, alisema kampuni hiyo yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 100 katika sekta ya ujenzi imekuja nchini kutafuta fursa za uwekezaji, akionesha kuvutiwa na maeneo yaliyowasilishwa na TBA pamoja na nia ya kuendeleza ushirikiano.
Aidha, alieleza uwezekano wa ushirikiano katika kujenga uwezo wa wataalamu (Capacity Building), mafunzo, usanifu majengo, teknolojia za ujenzi na usimamizi wa miradi, akizingatia uzoefu na maendeleo ya Japan katika sayansi na teknolojia.
Kikao hicho kilifuatiwa na ziara ya eneo la Canadian Village, Masaki, jijini Dar es Salaam, ambapo ujumbe wa Fujita Corporation ulijionea fursa za uwekezaji na uwezekano wa kushirikiana na TBA katika kuliendeleza.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuvutia mitaji, utaalamu na teknolojia kutoka Japan, kuongeza thamani ya rasilimali za TBA na kuchangia ukuaji wa uchumi.
TBA inaendelea kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa za uwekezaji zilizopo katika maeneo yake nchini.