Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

TBA YAONESHA MCHANGO WAKE KATIKA SEKTA YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KWENYE MAONESHO YA NANENANE 2025

Imewekwa: 03 August, 2025
TBA YAONESHA MCHANGO WAKE KATIKA SEKTA YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KWENYE MAONESHO YA NANENANE 2025

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeendelea kuonesha dhamira yake ya kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo ya sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kupitia miradi mbalimbali inayotekeleza, sambamba na kushiriki kwake katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

TBA imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia na kutekeleza miradi ya kimkakati inayochangia ustawi wa sekta ya kilimo nchini.

Kupitia Maonesho haya, TBA inaonesha namna inavyoshiriki katika kuboresha miundombinu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Miongoni mwa miradi mikubwa iliyoisimamia ni pamoja na Ujenzi wa Maghala na Vihenge vya kisasa vya kuhifadhi mazao ya kilimo katika mikoa nane nchini.

Mradi huo wa kihistoria umetekelezwa katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Manyara, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Njombe na Katavi, ukiwa na lengo la kuongeza uwezo wa Taifa katika kuhifadhi chakula na kudhibiti upotevu wa mazao baada ya mavuno. Ujenzi wa baadhi ya maghala hayo umekamilika na tayari umeanza kutoa huduma kwa wakulima na wanunuzi wa mazao.

Katika sekta ya Uvuvi, TBA imeonesha ubunifu kwa kuandaa na kusimamia mradi wa uzalishaji wa vifaranga vya samaki wa maji chumvi katika eneo la Ruvula (Msimbati), mkoani Mtwara. Sambamba na hilo, wakala pia umetekeleza usimamizi katika ujenzi wa mabwawa ya kufugia samaki katika eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam, miradi ambayo inalenga kuongeza uzalishaji wa samaki nchini na kuimarisha lishe pamoja na kipato cha wananchi.

Aidha, katika kuunga mkono sekta ya Mifugo, TBA imeshiriki katika ujenzi wa Soko la kisasa la mnada wa Upili wa mifugo katika eneo la Buzirayombo, mkoani Geita. Soko hilo ni kichocheo kikubwa cha biashara ya mifugo kwa wakulima na wafugaji wa Kanda ya Ziwa.

Wananchi mbalimbali wanaotembelea banda la TBA katika maonesho hayo wanapata fursa ya kujionea mchango wa wakala si tu katika ujenzi wa majengo ya umma, bali pia katika miradi ya kimkakati inayogusa maisha ya wananchi wa kawaida vijijini na mijini.

Maonesho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: "Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi," kaulimbiu inayobeba dhamira ya kuimarisha sekta hizo kwa ushirikiano wa wadau wote, wakiwemo TBA.