TBA YAANZA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeanza mkutano wa mwaka wa Baraza la Wafanyakazi, mkutano wa siku mbili unaolenga kujadili masuala muhimu ya utendaji na mustakabali wa Wakala.
Mkutano huo ulioanza leo Desemba 02, 2025 katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam, umefunguliwa na mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Wizara ya Ujenzi, Qs. Mwanahamisi Kitogo, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eng. Balozi Aisha Amour.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Qs. Kitogo amesema Serikali inaendelea na jitihada za kufungua sekta ya majengo kupitia marekebisho ya sheria na sera mbalimbali, hivyo TBA inapaswa kuongeza ufanisi na uwajibikaji, sambamba na kuimarisha mifumo ili isomane kwa urahisi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ubunifu katika majengo, hatua itakayowezesha TBA kushindana na kupata fursa zaidi katika miradi ya ujenzi.
"Ili kuleta ushindani katika soko, ni muhimu wataalamu wa TBA kuja na ubunifu mpya katika majengo tunayoyabuni, ili kufungua milango ya kunufaika na miradi mingi zaidi," amesema.
Pia amempongeza Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, pamoja na watumishi wote kwa maandalizi na uratibu mzuri wa Baraza hilo, ambalo limeendelea kuwa chachu ya utekelezaji wa majukumu ya Wakala kwa viwango vya juu vya ubora.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Kondoro amesema Baraza hilo ni jukwaa muhimu la kutathmini mafanikio, kujadili changamoto na kuweka mikakati ya pamoja kwa maendeleo ya taasisi.
Ameongeza kuwa TBA itaendelea kuendesha vikao vya Baraza la Wafanyakazi kwa kuzingatia weledi, uadilifu na uwajibikaji, sambamba na kufuata sheria, kanuni na miongozo ya usimamizi wa taasisi za umma ili kuhakikisha utoaji wa huduma bora.