TBA KUENDELEA KUSIMAMIA MILIKI ZA SERIKALI, KUJENGA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU.
Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) itaendelea kusimamia miliki za Serikali kwa lengo la kutoa makazi bora kwa viongozi pamoja na watumishi wa umma nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega wakati akiwasilisha makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma.
Waziri Ulega amesema Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza dhamira ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora na yenye gharama nafuu, hususan kwa vijana na wananchi wengine.
Amesema Wizara ya Ujenzi kupitia TBA imejipanga kukamilisha ujenzi wa nyumba 144 za gharama nafuu katika eneo la Temeke jijini Dar es Salaam, huku utekelezaji wa mradi mwingine wa nyumba 144 ukitarajiwa kuanza jijini Dodoma.
Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amesema Serikali itaendelea kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP) ili kuiwezesha TBA kujitegemea zaidi katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba na majengo mbalimbali.
Aidha, amesema Serikali kupitia TBA ipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa ubia (PPP) katika eneo la Temeke Kota jijini Dar es Salaam.
Pia, TBA imeainisha maeneo 149 katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara kwa ajili ya kuendelezwa kupitia miradi ya ubia. Baadhi ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji huo ni pamoja na Magomeni Kota na Masaki jijini Dar es Salaam.
“Tunawakaribisha wadau mbalimbali kushirikiana na TBA katika uwekezaji wa ujenzi wa majengo ya kupangisha kwa ajili ya Watanzania,” amesema Waziri Ulega