Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

TBA KUANZISHA DAWATI MAALUM LA DIASPORA KUKUZA UWEKEZAJI WA NYUMBA

Imewekwa: 24 January, 2026
TBA KUANZISHA DAWATI MAALUM LA DIASPORA KUKUZA UWEKEZAJI WA NYUMBA

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) uko katika hatua za mwisho za kuanzisha Dawati Maalum la Diaspora - (Watanzania wanaoishi nje ya nchi) lenye lengo la kuvutia na kurahisisha uwekezaji wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi katika sekta ya nyumba.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, amesema kuwa kuanzishwa kwa dawati hilo ni sehemu ya mikakati ya TBA katika kuimarisha miradi ya ubia, hususan ujenzi wa nyumba zitakazoendana na mahitaji na matarajio ya Watanzania waishio nje ya nchi.

Arch. Kondoro ameongeza kuwa TBA tayari imetambua na kutenga maeneo muhimu katika mikoa mbalimbali ambayo kwa sasa yanatangazwa rasmi kwa ajili ya uwekezaji, ikiwa ni pamoja na miradi itakayolenga kundi la Diaspora.

Hatua hiyo inalenga kuchochea uwekezaji, kuongeza upatikanaji wa makazi bora na kuimarisha mchango wa Diaspora katika maendeleo ya sekta ya nyumba nchini.