TBA YATUMIA NANENANE KUVUTIA WAWEKEZAJI WA SEKTA YA KILIMO
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) unatumia Maonesho ya Kilimo Nanenane kuwakaribisha wawekezaji katika sekta za kilimo, uvuvi na mifugo kuwekeza katika maeneo 38 ya kimkakati yaliyotangazwa na wakala huo katika mikoa 20 nchini.
Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TBA, Amina Lumuli, amesema hayo wakati akizungumza katika banda la TBA kwenye Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema TBA ina uzoefu mkubwa katika kubuni na kusimamia utekelezaji wa miradi ya kilimo, ikiwemo kubuni jengo la Wizara ya Kilimo pamoja na kusimamia ujenzi wa maghala ya kisasa ya kuhifadhia chakula katika mikoa minane nchini.
Kwa mujibu wa Amina, TBA ipo tayari kushirikiana na sekta binafsi katika kuendeleza miradi ya kilimo kupitia ujenzi wa maghala ya kisasa ya kuhifadhia mazao.
“Uhifadhi wa mazao unaongeza thamani ya mazao. Kabla ya kufika sokoni, mazao yanapaswa kuhifadhiwa katika maeneo salama na yenye viwango, hususan maghala ya kisasa. Tunakaribisha sekta binafsi kushirikiana nasi katika kujenga maghala ya kuhifadhia chakula,” amesema Amina.
Aidha, amesema baadhi ya maeneo 38 yaliyotangazwa na TBA yanafaa kwa uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, jambo litakalosaidia kuongeza tija katika sekta hiyo na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.
TBA imeendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kuonesha fursa za uwekezaji na kushirikisha wadau mbalimbali katika maendeleo ya miradi ya kimkakati inayolenga kuimarisha uchumi wa nchi.