Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

TBA YAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUSHIRIKI MIRADI YA NYUMBA ZA BIASHARA

Imewekwa: 07 August, 2025
TBA YAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUSHIRIKI MIRADI YA NYUMBA ZA BIASHARA

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeutumia vyema uwepo wake katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma kwa mwaka huu, kwa kuonesha miradi mbalimbali ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa na pia kutoa wito kwa wawekezaji kutoka sekta binafsi kushirikiana nao katika miradi ya nyumba za biashara nchini.
Akizungumza katika banda la TBA, Meneja wa TBA mkoa wa Dodoma, Qs. Emmanuel Wambura amesema, mbali na kuonesha mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, wakala huo unatumia maonesho hayo kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi kupitia mfumo wa ubia (PPP) katika ujenzi wa nyumba na miundombinu mingine ya kibiashara.
“Maonesho ya mwaka huu yamekuwa ya kipekee kwa TBA. Tumekuja na sera ya PPP – kushirikiana na sekta binafsi katika miradi ya ujenzi wa nyumba, na pia tunashirikiana na taasisi mbalimbali za serikali kwa mfumo wa Government to Government (G2G),” ameeleza Qs. Wambura.
Amebainisha kuwa maeneo ya kimkakati yaliyoainishwa kwa ajili ya uwekezaji katika nyumba za biashara ni pamoja na Canadian Masaki jijini Dar es Salaam, Ghana Kota jijini Mwanza, Kaloleni jijini Arusha na eneo la Kilimani jijini Dodoma. Ameongeza kuwa maeneo hayo tayari yameandaliwa kwa ajili ya uwekezaji, hivyo amewakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza kwa ushirikiano na TBA.
Katika maonesho hayo, TBA pia inaonesha mchango wake katika sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo kwa kuendelea kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa vihenge na maghala ya kuhifadhi chakula katika mikoa nane nchini. Vilevile, imefanya ubunifu wa mradi wa ujenzi wa mabwawa ya kufugia samaki wa maji chumvi katika mikoa ya Mtwara na Dar es Salaam.
Mbali na miradi hiyo, TBA imebuni na kutekeleza mradi wa ujenzi wa soko la mnada wa upili wa mifugo katika eneo la Buzirayombo mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuimarisha miundombinu ya masoko ya mifugo na kuunga mkono sekta ya mifugo nchini.