TBA MSHINDI WA PILI KATIKA KIPENGELE CHA SEKTA YA MILIKI KATIKA MAONESHO YA 50 YA KIMATAIFA YA BIASHARA YA DAR ES SALAAM (SABASABA)
Dar es Salaam, Julai 13, 2026 – Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeibuka mshindi wa nafasi ya pili na kutunukiwa tuzo katika kipengele cha Banda Bora upande wa Sekta ya Miliki (Real Estate) wakati wa hafla ya kufunga Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.
Tuzo hiyo imetolewa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na kupokelewa kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TBA na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi (DBS), Bi. Amina Lumuli.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, ambaye aliongoza sherehe za kufunga maonesho hayo na tuzo kutolewa kwa washindi wa makundi mbalimbali.
Ushindi huo unadhihirisha jitihada za TBA katika kuwasilisha huduma na miradi yake kwa ubora, pamoja na kuendelea kutoa mchango katika maendeleo ya sekta ya ujenzi na miliki nchini kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba.