WANAWAKE TBA WASHEREHEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Wanawake wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wameungana na wanawake wengine nchini kushiriki maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika leo Machi 8, 2026 katika mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Katika Mkoa wa Dar es Salaam, wanawake wa TBA walishiriki katika kilele cha maadhimisho yaliyofanyika katika Viwanja vya Mburahati Barafu vilivyopo Manispaa ya Ubungo. Vilevile wanawake wa TBA katika ofisi za mikoa mbalimbali nchini walijumuika na wadau wengine kushiriki maadhimisho hayo katika viwanja tofauti tofauti, wakionesha mshikamano na kuunga mkono juhudi za kuhamasisha haki na usawa wa wanawake.
Maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050.”
Ushiriki wa wanawake wa TBA unaonesha dhamira ya taasisi hiyo kuendelea kuunga mkono juhudi za kuwezesha wanawake na wasichana katika jamii.