Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YAFURAHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI INAYOTEKELEZWA NA TBA JIJINI DAR ES SALAAM

Imewekwa: 16 March, 2026
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YAFURAHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI INAYOTEKELEZWA NA TBA JIJINI DAR ES SALAAM

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeeleza kufurahishwa na kuridhishwa kwa kiwango kikubwa na utekelezaji wa miradi ya ujenzi inayosimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo ilitembelea na kukagua miradi hiyo Machi 14, 2026, katika ziara maalum ya ufuatiliaji wa maendeleo ya miradi ya Serikali. Katika ziara hiyo, wajumbe wa kamati walipata fursa ya kutembelea Mradi wa Nyumba za Makazi ya Magomeni Kota Awamu ya Pili pamoja na Mradi wa Nyumba za Makazi Canadian Masaki, Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso (Mb), aliipongeza TBA kwa kazi nzuri ya kutekeleza miradi hiyo kwa ubora, kuzingatia viwango vya ujenzi na kusimamia vyema rasilimali za umma.

Alisema kamati imevutiwa na maendeleo ya miradi hiyo pamoja na ubora wa majengo yanayojengwa, jambo linaloonesha dhamira ya Serikali katika kuboresha sekta ya makazi nchini.

Hata hivyo, Mhe. Kakoso aliishauri TBA kuendelea kubuni na kutekeleza miradi ya nyumba za makazi yenye gharama nafuu ili kuwapa fursa wananchi wa kipato cha chini kumudu makazi bora na salama.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb), alisema Serikali itazingatia na kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na kamati hiyo ili kuhakikisha miradi yote ya ujenzi inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi, ubora na kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaendana na maono na dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora, salama na yenye hadhi.