Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA)

ZBA YATEMBELEA TBA KUJIFUNZA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU NA MIKAKATI YA KUJITEGEMEA KIFEDHA

Imewekwa: 19 October, 2026
ZBA YATEMBELEA TBA KUJIFUNZA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU NA MIKAKATI YA KUJITEGEMEA KIFEDHA

Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) umetembelea Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa lengo la kujifunza mifumo ya kiutendaji, usimamizi wa miradi na mikakati ya kuongeza mapato ya ndani ili kuimarisha uwezo wa kujitegemea kifedha.

Akizungumza wakati wa kuikaribisha timu ya ZBA katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya TBA jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa TBA, FRV. Said Rajab Mndeme (ndc), amesema TBA ipo tayari kushirikiana na ZBA kwa kutoa wataalamu pale watakapohitajika, ili kutoa mwongozo katika maeneo mbalimbali yanayolenga kuboresha utendaji wa Wakala huo.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ZBA kufanya uchambuzi wa hali halisi ya taasisi (Situational Analysis) ili kubaini uwezo na maeneo yenye changamoto, hatua itakayowasaidia kuweka mikakati sahihi ya kuboresha utendaji na kufikia malengo yao.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa ZBA, Bi. Riziki Salim, ameishukuru Menejimenti ya TBA kwa ushirikiano walioupata, akieleza kuwa ziara hiyo imewapa fursa ya kufanya uchambuzi wa hali halisi ya uendeshaji wa Wakala na kujifunza mikakati inayoweza kuwasaidia kuboresha utendaji na kujiendesha kwa ufanisi zaidi.

Aidha, timu ya ZBA imeeleza baadhi ya changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kupata mbinu za kukabiliana nazo.

Vilevile, timu hiyo imetembelea Miradi inayotekelezwa na TBA katika eneo la Magomeni Kota Jijini Dar es Salaam, ili kujionea maendeleo ya utekelezaji wa Miradi hiyo na kujifunza kuhusu usimamizi wa miradi ya ujenzi.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu kati ya TBA na ZBA, kwa lengo la kuboresha utendaji, kuongeza ufanisi na kuimarisha uwezo wa taasisi hizo katika kutekeleza majukumu yake.

slot gacor