Desemba 1, 2022 Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro amezindua Bodi ndogo za Zabuni za Kanda sita za TBA na alifungua mafunzo ya Bodi kuu, Bodi ndogo na Kitengo cha Manunuzi TBA, mafunzo hayo ambayo ni ya siku tatu yameanza tarehe 1 mpaka 3 Desemba mwaka huu katika ukumbu wa mikutano wa St. Gasper Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Arch. Kondoro amesisitiza wajumbe wa bodi hizo kutumia fursa ya mafunzo hayo kuongeza ufanisi na weledi.
"Kwa kushiriki mafunzo haya mtaweza kutekeleza kwa urahisi majukumu ya Wakala katika kusimamia Ununuzi wa Vifaa, Huduma na Kandarasi mbalimbali. Hivyo ni imani yetu kwamba kumalizika kwa mafunzo haya, kutakuwa si tu chachu ya utekelezaji wa majukumu ya Wakala bali tutaweka Dira na mwelekeo wa masuala ya msingi yenye matokeo makubwa yatakayotuongoza katika shughuli za Ununuzi na kuondoa mapungufu yote yaliyojitokeza huko nyuma ili tuweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi shupavu wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" amesema Arch.
Kondoro
Vile vile Arch. Kondoro amesema uwepo wa Bodi hizo ni kwa Muujibu wa Sheria za Manunuzi ya Umma.
" Bodi hizi zinaundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 31 (1) cha Sheria ya ununuzi wa Umma ya mwaka 2011 na Kanuni zake za mwaka 2013 kinachoeleza kuwa kila Taasisi ya Serikali inapaswa kuwa na Bodi ya Zabuni itakayosimamia Ununuzi wa Bidhaa, Huduma, Kandarasi na Uondoaji wa vifaa. Kwa lugha rahisi, Bodi ya Zabuni ni chombo muhimu ambacho kinahakikisha kuwa utekelezaji wa Mpango wa Ununuzi na matumizi bora ya rasilimali fedha katika usimamizi makini wa Miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala wa Majengo kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali" amesema Arch. Kondoro.
Aidha, Arch. Kondoro amewataka wajumbe wa Bodi hiyo kuweka juhudi na maarifa yote mpaka hapo mafunzo hayo yatakapo malizika.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kudumu kwa siku tatu ambapo yamehusisha wajumbe kutoka mikoa yote 26 Tanzania Bara ambayo TBA ina ofisi zake nchini.