Dodoma, 5 Mei 2025 – Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb), amewasilisha Bungeni Mpango na Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025/26 akiainisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi na ukarabati wa nyumba na majengo ya Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA). Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa nyumba za makazi ya watumishi wa umma katika maeneo mbalimbali nchini, pamoja na usimamizi wa ujenzi wa majengo ya Wizara 19 katika Mji wa Serikali, Mtumba – Dodoma.
Katika hotuba yake, Mhe. Ulega ameeleza pia kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Uanzishwaji wa Wakala wa Majengo kupitia Tangazo la Serikali Na. 595, ambayo sasa inaruhusu TBA kushirikiana na Sekta Binafsi, kujenga na kuuza au kupangisha nyumba kwa bei ya soko. “TBA imeainisha maeneo yaliyoiva kibiashara katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Mwanza kwa ajili ya kuyaendeleza kwa njia ya ubia na mikopo kutoka taasisi za kifedha,” amesema Waziri Ulega.
Aidha, Waziri Ulega ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kushirikiana na TBA katika kuendeleza sekta ya ujenzi wa makazi. “Hatua hii inalenga kupunguza changamoto za makazi kwa watumishi wa umma, kuongeza mapato ya Wakala, na kupunguza utegemezi wa Serikali,” amesisitiza Mhe. Ulega.