DC NYAMAGANA AIPONGEZA TBA KWA KUTEKELEZA MIRADI MKOANI MWANZA
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt. Philis M. Nyimbi
ameupongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutekeleza
miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Mwanza.
Akiongea juu ya ujenzi wa jengo la ofisi ya
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dkt. Nyimbi amesema TBA imejenga jengo zuri,
lililojengwa kitaalam ambalo hata kimuonekano wa ramani ni jengo linalovutia. Pia
Mhe. Nyimbi alisema jengo hilo lina nafasi kubwa inayokidhi mahitaji ya ofisi
kwa watumishi wote na hakuna tena changamoto ya muingiliano kama ilivyokuwa
awali. Pia ameishukuru Serikali kwa kuipa TBA jukumu la kujenga jengo hilo
kwani kukamilika kwake kumeleta mafanikio makubwa kwa Wilaya ya Nyamagana na
wakazi wote wa jiji la Mwanza.
Aidha, Kaimu Meneja TBA Mkoa wa Mwaza Arch.
Salum Kihelo amesema miradi inayotekelezwa Mkoani Mwanza ni pamoja na Ujenzi wa
jengo la huduma ya mama na mtoto katika hospitali ya Sekou Toure, ujenzi wa
jengo la ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Misungwi, ujenzi wa jengo la ofisi
ya Mkurugenzi Buchosa, ujenzi wa jengo la Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kanda
ya Ziwa, ujenzi wa jengo la Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana na ujenzi wa jengo la
nyumba ya makazi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza.
Vile vile Arch. Kihelo aliongeza kwa kusema kuwa,
katika utekelezaji wa miradi hiyo ofisi ya TBA Mkoa wa Mwanza inatoa na kupokea
ushirikiano mkubwa kutoka kwa washitiri.