Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni Arch. Ng’wilabuzu Ludigija ameungana na Mhe. Rais Dtk. John Pombe Magufuli kuipongeza TBA kwa kutekeleza kwa wakati mradi wa ujenzi ya ofisi ya Halmashauri ya Manispaa Kigamboni. Arch. Ludigija ameelezea manufaa makubwa ya uwepo wa jengo hilo la ofisi kwa watumishi wake kuwa umeongeza kasi ya utendaji na kurahisisha shughuli mbalimbali za kiofisi. Vilevile hakusita kueleza matarajio yake katika kuendelea kufanya kazi na TBA hasa katika ujenzi wa nyumba za watumishi ambazo ziliahidiwa na Mhe Rais siku ya hafla ya uzinduzi wa ofisi hiyo.
Vilevile Mkuu wa Kitengo cha Tehama katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni Ndugu Edwin Johson Owawa amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa fedha za kujenga ofisi kwani zimekuwa na tija na kuongeza ufanisi kupelekea mabadiliko chanya ya kiutendaji.
Aidha, Bi Eusebia Nicholaus Nagunwa mkazi wa Mji Mwema, Manispaa ya Kigamboni amefurahishwa na kukamilika kwa ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Manispaa na kusema kuwa wameepukana na changamoto nyingi ambazo zilikuwa zinawanyima haki yao ya msingi kupata huduma kwa wakati. Pia ameipongeza TBA kwa kujenga jengo kubwa na la kisasa kwa kuzingatia muda wa mkataba.