Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Sekta ya Ujenzi Mhe. Mha. Godfrey Kasekenya ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi katika eneo la Ghana kota jijini Mwanza.
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Sekta ya Ujenzi Mha. Godfrey Kasekenya ameipongeza TBA kwa kazi nzuri na zenye ubora inazoendelea kuzifanya katika maeneo mbalimbali kama vile Dar es salaam (Temeke Kota, Magomeni Kota na Canadian), Arusha, na sasa mkoani Mwanza (Ghana Kota).
Pia Mhe. Kasekenya ameiagiza TBA kuhakikisha inamaliza mradi huo kwa wakati, kuzingatia ubora, viwango na gharama nafuu ili kujenga makazi yenye ubora wa hali ya juu kwa sababu jengo hilo linajengwa na kusimamiwa na TBA.
Aidha, Mhe. Kasekenya ameitaka TBA kushirikiana na Sekta binafsi pindi maboresho ya sheria ya kuanzisha TBA yatakapopitishwa ili kuhakikisha inajenga majengo mengi na yenye ubora kwa sababu TBA ina maeneo mengi yaliyo wazi hivyo itaweza kujenga majengo mengi zaidi ili kuendelea kukabiliana na uhaba wa nyumba nchini.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Mwanza Mha. Moses Urio alisema utekelezaji wa mradi huo ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoitaka TBA kujenga nyumba za ghorofa ili kuchukua familia nyingi na kupunguza uhaba wa nyumba nchini.
Pia, Meneja Urio aliongeza kuwa mradi huo umeleta manufaa makubwa kwani umetoa ajira kwa mama lishe, mafundi na wanufaika takribani 70 kwa mwezi pamoja na kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali.
Ujenzi wa jengo hilo unatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kutumia fedha za ndani na pindi jengo hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua familia kumi na nne (14) pamoja na maduka 30 kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii kwa wakazi watakaoishi kwenye nyumba hizo.