Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundo Mbinu imeupongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa ujenzi unaozingatia ubora na wenye kukidhi viwango. Pongezi hizo zimetolewa na Kamati hiyo Machi 12, 2020 baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa majengo ya Mji wa Serikali awamu ya kwanza eneo la Mtumba jijini Dodoma yaliyobuniwa na kujengwa chini ya usimamizi wa TBA.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Moshi Kakoso (Mb) amesema mradi walioutembelea ni mradi wa kitaifa unaoridhisha na kukidhi viwango vinavyotakiwa.
Naye Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro ameiambia Kamati hiyo kuwa mji huo umebuniwa (design) na kujengwa chini ya usimamizi wa TBA na kusema kuwa ubunifu wa Mji wa Serikali awamu ya pili unahusisha majengo makubwa na unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2020 ambapo kutakuwa na aina tatu za majengo (design 3) kulingana na wingi wa watumishi kwenye kila Wizara.
Aidha wajumbe wengine wa kamati hiyo walitoa pongezi za dhati kwa Mtendaji Mkuu wa TBA kwa kufanya wasilisho zuri kuhusu ubunifu na usimamizi wa Mji wa Serikali awamu ya kwanza pamoja na ubunifu wa Mji wa Serikali awamu ya pili.