Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Mhe. Japhet Hasunga Mbunge wa jimbo la Vyawa Mkoani Songwe leo 25 Machi, 2022 imefanya ziara ya kutembelea mradi wa ujenzi wa Nyumba za Watumishi wa Umma eneo la Magomeni Kota
Katika ziara hiyo Kamati ilipata nafasi ya kutembelea Nyumba za Makazi za Magomeni Kota ambazo zilifunguliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo 23 Machi, 2022. Pia Kamati ilitembelea mradi wa soko la wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama Magomeni Kota Machinga Centre na eneo la maduka ya kisasa (Shopping Malls) ikiwa ni sehemu ya miradi inayotekelezwa na TBA kupitia fedha za mapato ya ndani pamoja na kukagua mradi wa ujenzi wa Nyumba za Makazi za Watumishi wa Umma ambalo ndilo lengo kuu la ziara ya kamati hiyo.
Katika wasilisho la mpango kabambe juu ya uendelezaji wa eneo zima la Magomeni Kota lililotolewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Daud Kondoro amesema serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imetoa jumla ya shilingi bilioni 4.9 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2022. Kupitia mpango kabambe huo kunatarajiwa kujengwa maghorofa 5 zenye sakafu 7 kila moja ambazo zitakuwa na uwezo wa kuchukua familia 16 kwa kila jengo. Uendelezaji wa eneo hili utasaidia kupunguza changamoto ya makazi kwa watumishi wa umma katika jiji la Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo Mhe. Hasunga ameipongeza TBA kwa kazi nzuri ya ujenzi wa Nyumba za Makazi za Magomeni Kota na kuongeza kuwa kamati imeridhishwa na ujenzi unaoendelea.