Watumishi wapya wa kada mbalimbali wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wameanza mafunzo elekezi ya siku tano yanayotolewa na Chuo cha Utumishi wa Umma.
Mafunzo hayo yanawahusu watumishi wa taaluma zote na yanalenga kuwaeleza wahusika kuhusu utaratibu za utendaji kazi Serikalini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daniel Mwakasungula amesema mafunzo hayo ni kwa mujibu wa sheria na yanalenga kuongeza tija katika utendaji wa majukumu mbalimbali ya Serikali.
“Kama ilivyo Kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi Na.4. wa mwaka 2005 kuhusu Mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wa Umma unaelekeza Wajibu na Umuhimu wa Wizara au Idara za Serikali kuhakikisha watumishi wote wanaoajiriwa kwa mara ya kwanza wanapatiwa mafunzo ya utendaji na utekelezaji kazi Serikalini yaani Mafunzo Elekezi" amesema Arch. Mwakasungula.
Vile vile Arch. Mwakasungula amesema kupitia mafunzo hayo elekezi ni dhahiri kuwa watumishi hao watakuwa na uelewa wa kutosha juu ya namna ya kuheshimu miongozo mbalimbali.
“Watumishi hawa watakaopewa mafunzo elekezi leo watakuwa wamepata uelewa wa kuwa na nidhamu, ufanisi, uadilifu, uwezo wa utendaji bora wa kazi katika utumishi wa umma” amesema Arch. Mwakasungula.
Pamoja na mambo mengine Arch. Mwakasungula alifungua rasmi mafunzo hayo elekezi kwa watumishi wapya wa TBA ambayo yanatarajiwa kufanyika kwa siku tano.