Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Arusha Mhandisi Juma O. Dandi, ameeleza baadhi ya Miradi ya maendeleo inayotekelezwa na TBA Mkoani Arusha ambayo inatarajiwa kuwa na tija kwa wakazi wa jiji la Arusha na watanzania kwa ujumla. Miradi hiyo inajumuisha miradi ya Ujenzi, Ushauri pamoja na Ukarabati. Miradi ya ujenzi inayotekelezwa na TBA Mkoani Arusha inajumuisha Ujenzi wa Maabara ya nguvu za mionzi katika eneo la Njiro na Ujenzi wa jengo la Kibiashara linalojengwa katika mtaa wa Simeon jijini Arusha lenye uwezo wa kutoa makazi kwa familia ishirini na mbili (22).
Miradi ya ushauri iliyoainishwa na Mhandisi Dandi inajumuisha Ujenzi wa jengo la utawala katika Chuo cha Misitu Olimotonyi pamoja na Ujenzi wa nyumba mbili za watumishi wa Mahakama zilizopo eneo la Wasso Wilayani Loliondo. Vile vile miradi ya ukarabati inayotekelezwa katika Mkoa wa Arusha ni pamoja na Ukarabati wa jengo la Maabara katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) kilichopo Tengeru na Ukarabati wa jengo la abiria katika Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA).
Aidha, Mhandisi. Dandi ameainisha mkakati wa kukamilisha ukarabati wa Karakana kufikia mwezi Juni, 2020. Mhandisi. Dandi alifafanua manufaa ya ukarabati wa karakana hiyo kuwa ni pamoja na kutatoa nafasi za ajira kwa vijana, kupunguza gharama za ujenzi kwa kutumia vifaa kama fremu za milango, madirisha na samani nyingine zitakazozalishwa na karakana hiyo kwa gharama za chini, pamoja na kuongeza mapato kwa kuuza bidhaa zitakazozalishwa na karakana.