Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametembelea eneo la Gezaulole, Manispaa ya Kigamboni na kuzindua rasmi jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni pamoja na jengo la Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni.
Mhe. Rais amefurahishwa na kuipongeza TBA kwa kukamilisha ujenzi wa ofisi hizo ambazo zitasaidia kutoa huduma kwa wananchi na kuongeza kasi ya maendeleo katika Wilaya ya Kigamboni kwa ujumla. Pia Mhe. Rais amempongeza Msimamizi wa Mradi, Arch. Edwin Godfrey kwa usimamizi mzuri uliopelekea miradi hii kukamilika kwa wakati.
Aidha, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro amemshukuru Mhe. Rais kwa kuridhishwa na kazi iliyofanywa na TBA katika kutekeleza miradi hiyo ya maendeleo. Pia ametoa rai kwa washitiri wengine kushirikiana na TBA kufanya kazi kama timu katika kutekeleza miradi hiyo.
Akiongea kuhusu kusifiwa na Mhe. Rais, Meneja wa TBA Mkoa wa Dar es Salaam Arch. Edwin Godfrey amesema anaichukulia kama changamoto inayompasa kuongeza bidii zaidi na ubunifu ili kuendana na matarajio ya Mhe. Rais.