Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ameteua wajumbe wanaounda Bodi mpya ya Zabuni ya Awamu ya nane na kuizindua rasmi. Bodi hiyo itakuwa na jukumu la kupitisha manunuzi yatakayofanyika kwenye Ofisi za TBA Makao Makuu pamoja na kusimamia utendaji wa Bodi ndogo za Zabuni za Kanda zinazojumuisha Kanda ya Pwani, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kusini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro ameitaka Bodi hiyo kufanya kazi kwa weledi ili kuongeza ufanisi na tija katika shughuli zote za ununuzi kwa kuzingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011 na Kanuni zake za mwaka 2013 kama zilivyorekebishwa mwaka 2016 na 2018.
"Ninamatarajio makubwa kuwa Bodi hii itatekeleza majukumu yake kwa weledi na maarifa ili kuwezesha kufikia malengo ya Wakala na Serikali kwa ujumla" amesisitiza Arch. Kondoro.
Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha Mtendaji Mkuu wa TBA, Meneja wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi Bibi. Mariam Kazoba alisema kuwa kumekuwa na manufaa mbalimbali kupitia uwepo wa Bodi hiyo ikiwa ni pamoja na TBA kufanikiwa kutekeleza shughuli za ununuzi kwa ufanisi na kufanikiwa kupata 89.11% kwenye Ukaguzi wa Thamani ya Fedha yaani Value for Money Audit uliofanywa na PPRA mwezi Septemba, 2022.
Bodi mpya ya Zabuni iliyozinduliwa itadumu kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia tarehe 1.07.2023 hadi 30.06.2026.