Agosti 05, 2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametembelea na kuweka jiwe la Msingi kwenye Mradi wa Ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya iliyobuniwa na kujengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Baada ya kuweka jiwe la msingi Mhe. Rais Samia amepongeza jitihada zilizochukuliwa katika utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa utakwenda kusaidia wakazi wa Mbeya kupata huduma bora za kiutawala.
Aidha Mhe. Rais Samia amesema amezunguka Mikoa mingi na kuona majengo ya Wakuu wa Mikoa mbalimbali lakini jengo la Mkuu wa Mkoa wa Mbeya lililobuniwa na kujengwa na TBA ni la aina yake kutokana na ubora na uzuri wa jengo hilo.
Hata hivyo, Mhe Rais Samia amesifia kazi nzuri ambayo imefanywa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika kuhakikisha shughuli ya Serikali ya Utawala Bora inatekelezwa vyema katika kuboresha maeneo ambayo wananchi wataweza kuhudumiwa.
Mhe. Rais pia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kujenga Majengo makubwa ya aina hiyo katika mikoa mbalimbali hasa maeneo ya Makao Makuu ya Kanda.
Akizungumza na TBC1 baada ya kuweka jiwe la msingi, Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuweka jiwe la msingi.
"Kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais Samia kuweka jiwe la msingi, hii inaashiria jengo limekidhi viwango vya ubora na utekelezaji wa Mradi huu kwa TBA ni wajibu kwa sababu Wakala una jukumu la kusimamia Miliki za Serikali ikiwemo Ofisi na nyumba za Serikali na kuhakikisha Watumishi wanakaa katika makazi ambayo ni salama ambayo yanaweza kuleta tija katika kutoa huduma" alisema Arch. Kondoro.
Akizungumza juu ya ubora wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa ya Mbeya Arch. Kondoro amesema kuwa TBA imefuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na kupima malighafi zote za ujenzi ili kujiridhisha na viwango vya ubora.
Aidha, Arch. Kondoro amezungumzia ushiriki wa TBA katika mradi wa ujenzi wa Mji wa Serikali katika eneo la Mtumba Jijini Dodoma."Unafahamu kuwa kuna ujenzi unaendelea sasa wa Mji wa Serikali awamu ya pili ambapo ubunifu wa mji ule umefanywa na TBA lakini pia tunajenga baadhi ya Majengo" alisema Arch. Kondoro.
Mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya unatekelezwa na TBA kama Mkandarasi na kusimamiwa na MUST kama Mshauri Elekezi ambapo uwekaji wa Jiwe la Msingi la ujenzi wa mradi huo umefanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Agosti 5, 2022.