Operesheni ya kuwaondoa wadaiwa sugu katika nyumba za Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), imeendelea kutekelezwa katika mkoa wa Dodoma. Utekelezwaji wake unahusisha kuwaondoa wadaiwa sugu, watu wanaoishi katika nyumba za TBA kinyume na utaratibu ambao si wapangaji halali pamoja na watu wengine waliojimilikisha mali za TBA zikiwemo nyumba na viwanja pasipo halali.
Akizungumzia zoezi hili, Kaimu Meneja wa TBA mkoa wa Dodoma Arch. Vilumba Sanga amesema, zoezi litakuwa endelevu hadi pale wadaiwa wote watakapokuwa wamelipa madeni yao.
"Pamoja na wadaiwa sugu lakini pia kuna baadhi ya wapangaji hawaishi kwenye nyumba hizo badala yake wameweka watu wengine wanaishi pasipo halali, kinyume na utaratibu unaotakiwa, tutawaondoa wote na madeni wanayodaiwa lazima wayalipe kwa mujibu wa mkataba" Amesisitiza Arch. Sanga
Aidha, Arch. Sanga, ametoa wito kwa wapangaji wote kuzingatia utaratibu wa kimkataba, kulipa kodi kwa wakati, kutolimbikiza kodi na kuachiana nyumba kiholela pasipo kufuata utaratibu.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Twins Auction Mart, ambao ndiyo walioshinda zabuni ya kuwaondoa wapangaji hao kwa taratibu za Mahakama, Bw. Zuberi Hassan, amebainisha kuwa zoezi linakwenda vizuri na watahakikisha kuwa wadaiwa wote wanaondolewa kwenye nyumba hizo na kulipa madeni yao.