Watumishi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wanaendelea kupatiwa mafunzo ya Mfumo mpya wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Mtandao (NeST).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TBA, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Bw. Mathias Mhembe amesema kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kupitia Waraka wa Hazina Na.2 wa mwaka 2023/2024 unaozitaka Taasisi Nunuzi zote hapa nchini kuanza mara moja kutumia mfumo mpya wa usimamizi wa ununuzi wa umma kwa njia ya kielektroniki (NeST) ifikapo Oktoba Mosi mwaka 2023.
Pia Bw. Mhembe amesema kuwa anatarajia kuwa mfumo huo mpya utatatua changamoto zilizokuwepo wakati wa matumizi ya mfumo wa ununuzi wa Taneps.
“Nimejulishwa kuwa, mfumo huu mpya unakwenda kutatua changamoto zote zilizokuwepo kwenye mfumo wa zamani ikiwemo ucheleweshaji wa michakato ya zabuni, upatikanaji wa wazabuni na watoa huduma wasiokidhi vigezo ama kutokuwa na uwezo wa kutekeleza kazi. Ni imani yangu kwamba kutokana na mabadiliko na kurahisishwa kwa teknolojia, mfumo huu mpya wa NeST utakuwa rafiki na utakidhi mahitaji ya sasa” amesema Bw. Mhembe.
Awali akitoa taarifa ya matumizi ya mfumo mpya, Mkurugenzi wa Mifumo ya Habari kutoka PPRA Bw. Michael Moshiro alisema kuwa mfumo mpya wa ununuzi wa NeST utaongeza uwazi na uwajibikaji ukilinganisha na mfumo wa ununuzi uliokuwepo wa Taneps.
Mafunzo ya Mfumo mpya wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Mtandao (NeST). yanatolewa kwa siku tano na maafisa kutoka PPRA kuanzia Septemba 11-15, 2023 mjini Iringa yakihusisha watumiaji wa mfumo kutoka Ofisi za TBA ambao ni Afisa Masuuli, Bodi ya Zabuni, Maafisa Ununuzi na Ugavi, Wakuu wa Vitengo na Sehemu, wawakilishi wa Idara tumizi, Wanasheria na Maafisa TEHAMA.