Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umesaini hati ya ushirikiano na Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) kwa lengo la kujifunza, kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu.
Hati ya makubaliano hayo upande wa TBA imesainiwa na Mtendaji Mkuu Arch. Daud Kondoro katika Mkutano wa mashauriano kati ya Serikali, Wakandarasi na Washauri Elekezi wa ndani uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Mashirikiano haya yamelenga zaidi katika kuimarisha ubadilishanaji wa ujuzi na maarifa kati pande hizi mbili na kusimamia kadri iwezekanavyo mfumo wa kudhibiti ubora, usimamizi wa miradi ya ujenzi wa majengo ya Serikali na kupata uzoefu zaidi.
Wataalamu wa pande zote mbili watatembelea miradi, kutoa ushauri na kujifunza kwa lengo la kuleta ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya Serikali.
Hadi makubaliano haya yanasainiwa, tayari baadhi ya wataalamu kutoka ZBA wameshafanya ziara ya kutembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa na TBA katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma ukiwemo mradi mkubwa wa kimkakati wa ujenzi wa Mji wa Serikali.