Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeendelea na mpango maalumu wa ukaratabati wa nyumba na majengo katika maeneo mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuboresha makazi na kuongeza ufanisi kwa Watumishi wa Umma ambao ndiyo wapangaji wa nyumba hizo. TBA imeendelea na jitihada hizo za ukarabati ambao unahusisha ukarabati wa paa, kupaka rangi, mifumo ya maji safi na taka Pamoja na ukarabati wa miundombinu ya umeme.
Mkoa wa Songwe ni miongoni mwa mikoa ambayo imenufaika na ukarabati huo ambapo ukaratabati unafanyika katika Wilaya ya Mbozi, kata ya Ichenjezya. Akizungumza juu ya ukarabati huo Afisa Miliki wa TBA Mkoani Songwe Bw. Thomas Mwasalyanda amesema katika eneo hilo kuna jumla ya nyumba kumi na mbili (12) ambazo zinabeba familia ishirini (20). “Ukarabati huu ulianza Februari, 2022 ambapo tulianza kufanya marekebisho ya paa, ikumbukwe pia hakukua na marumaru (tiles) katika maeneo ya jikoni, bafuni na chooni lakini kupitia ukarabati huu tumefanikisha kuweka marumaru. Vile vile tumefanikisha kuboresha miundombinu ya umeme ambapo kwa sasa kila nyumba imekuwa na mita ya luku pamoja na kuboresha upatikanaji wa maji ya uhakika kwa kuchimba kisima katika eneo hilo” amesema Mwasalyanda.
Vile vile Bw. Mwasalyanda amezungumzia juu ya ubora wa ukarabati huo ambapo amesema umezingatia taratibu zote katika maeneo yaliyofanyiwa ukarabati kwa kuondoa vifaa vyote vilivyokuwa vimechakaa na kuweka vifaa vinavyokidhi viwango vya ubora na ambavyo vitadumu kwa muda mrefu zaidi.
Bibi Mariam Shaban ni miongoni wa wakaazi wa eneo wa hilo ambaye amezungumzia ukarabati huo "kwa kweli tumefurahi kwa kufanyiwa ukarabati huu kwa sababu nyumba zinavyoonekana sasa ni tofauti na zilivyokuwa awali. Lakini jambo kubwa tunaloweza kuishukuru TBA ni kutuwekea maji ya uhakika kwa kuchimba kisima ambacho kinasambaza maji katika nyumba zote hizi na maji hayo yanapatikana wakati wote” amesema bibi Mariam.
Utekelezaji wa mpango wa ukarabati katika Wilaya Mbozi, kata ya Ichenjezya kwa sasa umefikia asilimia 80 za utekelezaji ambapo kazi mbalimbali zimekamilika. Vile vile ukarabati huo unatarajia kuendelea kufanyika katika wilaya ya Ileje katika Mkoa huo wa Songwe kwa lengo la kuboresha makazi ya watumishi wa umma.