Wakala
wa Majengo Tanzania (TBA), umeahidi kusaidia Ujenzi na Ukarabati wa Majengo
katika Shule ya Sekondari Juhudi iliyopo
eneo la Gongo la Mboto, Ilala Jijini Dar es Salaam. Shule hiyo iliyoanzishwa na
kuendelezwa na wananchi wa eneo hilo, inakabiliwa na uchakavu wa miundo mbinu
ya majengo kama ofisi na madarasa, hivyo kuwafanya wanafunzi na walimu kusoma
na kufanya kazi katika mazingira magumu.
Akizungumza
katika Mahafali ya Tatu ya Kidato cha Sita baada ya kusikiliza Risala
iliyosomwa na Mkuu wa Shule pamoja na Risala iliyosomwa na viongozi wa Serikali
ya Wanafunzi, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TBA Bw. Said Mndeme aliyekuwa Mgeni Rasmi
katika Mahafali hayo alisema, “TBA kama mdau wa sekta ya elimu upande wa miundo
mbinu ya majengo na majenzi tutakarabati majengo ya Utawala na Ofisi za walimu
pamoja na Madarasa 10 ya wanafunzi”. Pia aliahidi kujenga Ofisi kwa ajili ya
serikali ya wanafunzi ambao wanafanya kazi bila kuwa na ofisi kwa sasa.
Shughuli
ya Ukarabati imeshaanza kwa hatua za awali kwani mgeni rasmi aliambatana na
jopo la wataalamu kutoka TBA ambao kabla ya kuanza kwa mahafali walitembelea na
kuanza kufanya tathmini ya majengo yanayohitaji ukarabati.
Shule ya Sekondari Juhudi inaibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi katika Sekta ya Michezo lakini inakabiliwa na changamoto ya kukosa viwanja na miundo mbinu mingine ya michezo. Katika sherehe hizo za mahafali Mgeni Rasmi aliahidi kulifikisha suala hilo kwa wadau mbalimbali wa michezo ili walishughulikie.