WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) unatekeleza mradi ujenzi wa nyumba 3500 za makazi kwa ajili ya watumishi wa umma katika eneo la Nzuguni B jijini Dodoma. Mradi huo ambao unatekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza zimejengwa yumba 150 ambazo zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi na umaliziaji.
Akitoa ufafanuzi juu ya utekelezaji wa mradi huo Msimamizi wa mradi huo Arch. Fedrick Jackson amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza Oktoba 25, 2021 na unatarajiwa kukamilika Septemba 30, 2022 ambapo hadi sasa umefikia asilimia 70 za ujenzi ambapo nyumba 102 zimefikia hatua ya umaliziaji na nyumba 48 zipo hatua mbalimbali za ujenzi.
Arch. Fedrick ameendelea kusema kuwa nyumba zilizojengwa katika eneo hilo ni za chini zenye ukubwa mita za mraba 100 ambapo ukubwa wa kiwanja ni mita za mraba 600. Akielezea sifa za nyumba hizo Arch. Fedrick amesema nyumba hizo zina vyumba vitatu vya kulala, sebule, jiko na stoo. Pia amesema nyumba hizo zina sehemu ya kuegesha gari (car parking), sehemu ya kuchezea watoto, sehemu za kupumzika pamoja na eneo kwa ajili ya bustani za maua (garden).
Pamoja na mambo mengine Arch. Fedrick amesema kazi mbalimbali zinaendelea katika utekelezaji wa mradi huo ambapo kwa sasa wanaendelea na kazi za upigaji rangi kwa nyumba zilizo hatua ya umaliziaji, ufungaji wa vifaa vya umeme, ufungaji wa mabomba ya mifumo ya maji safi na taka pamoja na uendelezaji wa nyumba arobaini na nane (48) ambazo zipo katika hatua ya ujenzi. Pia tunaendelea kupanda miti kwa lengo la kuboresha mazingira na kuunga mkono kauli mbiu ya Dodoma ya kijani kwa kupanda miti alisema Arch. Fedrick.
Katika kuzingatia viwango vya ubora Arch. Fedrick amesema tangu walipoanza mradi huo, katika hatua ya awali wanapima malighafi zote za ujenzi na kujiridhisha kabla ya kuvitumia pamoja na kuwa timu maalum ambayo imekuwa ikijiridhisha na ubora kwa hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo.
Mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 katika eneo la Nzuguni B unatekelezwa na TBA kama Mkandarasi na Mshauri Elekezi ambapo kwa awamu ya kwanza zimeshaanza kujengwa nyumba 150 ambazo zinatarajiwa kukamilika Septemba 30, 2022.
Mradi huu utakapokalimilika unatarajiwa kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba za makazi kwa watumishi wa umma jijini Dodoma pamoja na kuongeza ufanisi kwa Watumishi wa umma.